DK. SHEIN: WANANCHI ACHENI UKAIDI, FATENI MAELEZO YA SERIKALI.
#ZANZIBAR :-
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kuacha ukaidi na kufuata kikamilifu maelekezo ya Serikali, ikiwa ni hatua za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na Virusi vya Ugonjwa wa Corona.
Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipotembelea eneo linalotarajiwa kujengwa jengo la Uchunguzi wa maradhi makuu, liliomo ndani ya taasisi ya Utafiti wa Afya, huko Binguni, Wilaya Kati Unguja.
Amesema katika kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo, Serikali tayari imetowa malekezo kadhaa, ikiwa njia ya kujikinga na virusi vya ugonjwa huo, hivyo akawataka wananchi kuacha ukaidi na kutekeleza maelekezo ya kudumisha usafi kama inavyoelekezwa.
Alisema Virusi vya Ugonjwa wa Corona ni janga na Kimataifa na ni maradhi yasiotaka mzaha wala hayachaguwi aina ya mtu wa kuamuathiri, hivyo ni vyema wananchi wakaondokana na ushindani na kuzingatia maelekezo ya Serikali.
Alieleza kuwa Serikali imeingia katika vita dhidi ya adui asieonekana na hivyo ikalazimika kuchukuwa hatua mbali mbali za dharura ikiwemo kuzuia Kongamano la dini pamoja na kuzifunga skuli zote na wanafunzi kukosa taaluma.




Comments
Post a Comment